Monday, August 12, 2013

THE VOICE OF THE VOICELESS WOMAN

Bwana asie na jema,ni madhila kumpata
Mahaba nayo mema,bado wala hajapata
Akuona mgema,ye mlevi aja pata
Madhila siniletee,afriti jiendee

Bangi kwake ni rehema,kuacha shari apata
Pombe kwake ndio mama,akilewa  kero napata
Kwenye simu atukama,kesho radhi anapata
Madhila siniletee,afriti jiendee

Kwa sengenyo na zahama,pesa yake kuipata
Majirani waachama,kipigo mke napata
Kila nyumba twahama,pango shida kulipata
Madhila siniletee,afriti jiendee

Wana natunza mama,baba pesa hajapata
Zote wampa mgema,aila dhiki twapata
Wanao kama yatima,mitaa kutwa wakata
Madhila siniletee,afriti jiendee

Wanisaidia mama,riziki japo kupata
Wikiendi na rukwama ,michezo mwiko kupata
Leo mimi nakuhama,kamwe hautoukata
Madhila siniletee,afriti jiendee

Shule mie nilisoma,kibarua nitapata
Maishani sitokwama,za mola Baraka tapata
Mume talaka nataka,nimechoka namadhila
Madhila siniletee,afriti jiendee



No comments:

Post a Comment